Serikali ya Tanzania imeagiza kufanyika kwa uchunguzi kuhusu kanda ya video ilioonyesha kundi moja la walimu likimpiga mwanafunzi.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo ya sekondari ya kutwa ya Mbeya tayari amesimamishwa kazi kwa muda kwa kutochukua hatua hata baada ya kugundua kuhusu kisa hicho, taarifa ya serikali imesema.
"Nimesikitishwa kwa kitendo cha mwalimu mkuu wa shule hiyo ndugu Magreth Haule kutochukua hatua zozote ikiwa ni pamoja na kotukutoa taarifa hadi leo tulipoona kwenye mitandao ya kijamii," alisema waziri wa ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) George Simbachawene, kupitia taarifa.
"Hii inaonesha kulikuwa na dalili ya kutaka kulificha tukio hili baya. Na kwa sababu hiyo pamoja na kwamba wanaendelea kuhojiwa na polisi, naagiza mamlaka ya nidhamu, kumvua madaraka mkuu huyo wa shule."
Raia wa Tanzania katika mitandao ya kijamii walionyesha hasira zao, wakiitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya washambuliaji hao.
Video hiyo ambayo haijakaguliwa inaonyesha mwanafunzi mmoja akipigwa na kundi la walimu katika kile kinachoonekana kuwa chumba cha wafanyikazi wa shule.
Katika kanda hiyo ya sekunde 38, takriban watu watano wanaonekana wakikabiliana na kushambulia mvulana huyo aliyeanguka chini kwa kumpiga ngumi pamoja na mateke.
Adhabu ya kupigwa viboko ni haramu nchini Tanzania,na kisa hicho cha hivi karibuni kinatarajiwa kuzua mjadala kuhusu utekelezwaji wa sheria hiyo katika shule za taifa hilo.
bbc
Post a Comment