Unknown Unknown Author
Title: NAMNA YA KUONDOKANA NA ULEVI WA MICHEZO YA KAMARI NA HATA MITANDAO YA KIJAMII
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Yafuatayo ni mambo muhimu kufanya ili kuondokana na ulevi wa michezo, kamari na hata mitandao ya kijamii.  1. Kubali kwamba una tatizo.  Ha...
 MAMBO MATANO (5) MUHIMU KUFANYA ILI KUONDOKANA NA ULEVI WA MICHEZO, KAMARI NA HATA MITANDAO YA KIJAMII.
Yafuatayo ni mambo muhimu kufanya ili kuondokana na ulevi wa michezo, kamari na hata mitandao ya kijamii. 

1. Kubali kwamba una tatizo. 

Hatua ya kwanza kabisa ya kutatua tatizo hili la ulevi ni kukubali kwamba una tatizo. Kwa sababu usipokubali una tatizo, huwezi kukubali msaada wowote. Kubali kwamba kuna vitu ambavyo umekuwa unafanya kwa muda mrefu ambavyo vimekuwa havina msaada wowote kwako. Kubali kwamba matumizi yako ya mitandao ya kijamii yamevuka kiasi. 

2. Badili marafiki. 

Ukiangalia kwa makini, utagundua marafiki zako nao ni wateja wa kile ambacho na wewe umeshakuwa mteja. Hii ina maana kwamba unapokutana na marafiki zako, wote mnawaza kitu kimoja, ambacho ni ule ulevi wenu. Unahitaji kubadili marafiki ulionao, au kupunguza muda na marafiki ambao unao. Hii itakupa nafasi ya kuweza kukaa mbali na kile ambacho tayari umeshakuwa na ulevi nacho. 

3. Tafuta kitu kingine ambacho kitakuweka ‘bize’. 

Unapotaka kuacha ulevi wowote ulionao sasa, ni vyema ukapata kitu ambacho kitakuweka bize. Kama utaacha halafu ukawa huna kitu kingine cha kufanya, itakuwa rahisi kwako kurudi kwenye tabia uliyoacha. Unapopata kitu kingine cha kufanya, akili na mawazo yako yote yanakuwa kwenye kitu hicho kipya na hivyo kuwa rahisi kusahau ule ulevi wako. 

Tafuta kitu ambacho unapenda kufanya, ambacho kitakuondoa kwenye ulevi ulionao sasa. Inawezekana ikawa kujifunza, au kazi fulani unayoipenda sana. Kila unapopata mawazo ya kwenda kufanya kile ambacho una ulevi nacho, fanya kile ulichopanga kufanya. 

4. Epuka vishawishi vya kurudia ulevi unaotaka kuachana nao. 

Mara nyingi unaweza kujipanga vizuri kuacha kitu fulani, lakini vishawishi vikawa vingi na kujikuta unarudia kile unachotaka kuacha. Moja ya vishawishi ni marafiki, ambao tumeshawazungumzia hapo juu. 

Vishawishi vingine ni mazingira, kama upo kwenye mazingira ambayo yanahamasisha tabia fulani, inakuwa vigumu kwako kuiacha. Kama upo kwenye mtaa ambao kila mtu anacheza mchezo fulani unaotaka kuacha, itakuwa vigumu kwako. Kama simu yako ina mitandao ya kijamii ni vigumu kwako kuondokana na ulevi huu. 

Badili mazingira yako ili yakuweke mbali na vilevi vyovyote unavyotaka kuachana navyo. 

5. Pata msaada wa kuweza kuondokana na ulevi wowote ulionao. 

Kama njia zote hapo juu hazitakusaidia, basi ipo njia ya uhakika ya kukuwezesha kuachana na ulevi wowote unaokusumbua. Njia hii ni kupata msaada wa wengine. Kupata msaada kupo kwa aina mbili. 

Aina ya kwanza ni kujiunga na vikundi vya watu ambao wanataka kuachana na ulevi ambao na wewe unataka kuachana nao. Kwa kuwa kwenye vikundi hivi mara kwa mara mnakutana na kujadili changamoto mbalimbali na njia bora ya kufikia malengo yenu. 

Aina ya pili ni kuwa na mshauri ambaye atakuwa anakusimamia katika hilo unalofanya. Mtu huyu atakufuatilia kwa karibu kuhakikisha kweli umeachana na tabia hiyo ambayo siyo nzuri kwako. 
Maisha bora na yenye mafanikio ni yale maisha ambayo yana uhuru wa mwili na akili. 

Unapokuwa na ulevi wa kitu chochote, tayari unakuwa umepoteza uhuru wako, maisha yako hayawezi kuwa bora na huwezi kuwa na mafanikio. Kama kuna ulevi wowote ambao unakusumbua kwa sasa, hakikisha unaondokana nao. Utajuaje kitu ni ulevi kwako? Kama unashindwa kujizuia kufanya, basi umeshakuwa mlevi. 

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top